MFANYA BIASHARA DAWA ZA ASILI AFUNGIWA KWA KUUZA DAWA ZINAZOPASWA KUUZWA PHARMACY
Na Fauzia Mussa, Zanzibar
BARAZA la Tiba asili na tiba mbadala Zanzibar, kwa kushirikiana na
Wakala wa chakula na Dawa (ZFDA), wamelifungia duka la dawa asili maeneo ya kwa
Hajitumbo kutokana na kuwepo kwa dawa za hospitali katika duka hilo.
Hayo yamebainika kufuatia ukaguzi uliofanywa na baraza hilo katika
baadhi ya maduka yaliopo mkoa wa Mjini Magharibi.
Mrajisi wa baraza la Tiba asili na tiba mbadala
Zanzibar,Mohammed Mshenga Matano akizungumza na waandishi wa habari baada
ya ukaguzi huo alisema kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Aidha alieleza kuwa baraza haliridhishwi na tabia ya
wafanyabiashara kama hao wanaochanganya dawa za asili na dawa
za hospitali kwani mbali ya kwenda kinyume na sheria lakini pia wanahatarisha
afya za jamii.
“Katika duka hili tumebaini uwepo wa dawa
zisizostahiki kuuzwa hapa, kwani muuzaji hawezi kutoa maelezo
sahihi ya kutumia dawa hizi zinazoelekeza zitumiwe kwa mujibu wa
maelekezo ya daktari” Alisema
Alisema uzowefu unaonesha kuwa wafanyabiashara wengi wa dawa
za asili hawana utaalamu wa dawa za hospitali, hivyo endapo dawa hizo
zitatolewa bila muongozo wa daktari zitaleta athari kwa mtumiaji.
Mbali na hayo alieleza kuwa baadhi ya dawa hizo
zimemaliza muda wa matumizi na kutoa wito kwa jamii kutumia dawa kwa ushauri na
maelekezo ya daktari ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Alizitaja baadhi ya dawa zilizobainika katika duka
hilo kuwa ni pamoja na dawa za kuongeza nguvu za kiume, pamoja na
za kutibu magonjwa ya wanawake ambazo zote zinahitaji muongozo wa daktari
wakati wa kuzitumia.
Alisema licha ya Baraza hilo kuchukua juhudi ya kuwapatia
elimu watoa huduma za tiba mbadala wakati wa ukaguzi lakini bado baadhi
ya wadau hao wanaendesha biashara hiyo kinyume na taratibu zilizowekwa.
Alieleza Kwa mujibu wa sheria namba nane ya mwaka 2008 ya
baraza hilo hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa makosa kama hayo ni pamoja
na kuziondoa sokoni dawa hizo,au kutozwa faini isiyopungua laki
moja na isiyozidi laki mbili, au kifungo kisichopungua mwezi mmoja na kisichozidi
miezi 6, au adhabu ya kusitisha huduma hadi taratibu zitakapokamilika au vyote
kwa pamoja.
Mkuu wa divisheni ya vipodozi walala wa dawa na chakula (ZFDA),
Mfamasia Salim Hamad Kassim alisema wataendelea kushirikianana na
baraza la tiba asili na tiba mbadala ili kuondoa changamoto hizo na
kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Alifahamisha kuwa endapo dawa za hospitali
zitahifadhiwa vibaya au kuingizwa nchini bila utaratibu unaokubalika kutaleta
athari moja kwa moja kwa mtumiaji wa miwsho, hivyo ZFDA itashirikiana na kila
mdau katika kulinda afya za wananchi.
Hata hivyo alilishukuru baraza hilo kwa ukaguzi wao uliosaidia
kuibua maovu ya wadau wa tiba asili dhidi ya jamii, na kuishauri jamii
kuacha kununua na kutumia dawa kiholela ili kulinda afya zao .
Mmiliki wa duka hilo Mwatima Bakari Mussa alikiri kufanya
kosa hilo na kuiomba radhi Serikali na jamii kwa ujumla
kutokana na makosa hayo aliyodai kufanywa bila kujua.
Alifahamisha kuwa duka hilo limekua likipokea dawa kutoka sehemu
mbalimbali bila kuangalia uhalali na ubora wake, hivyo aliiahidi kuwa makini
wakati wa kupokea dawa hizo ili kuepusha kutokea tena kwa makosa kama
hayo dukani hapo.
Baadhi ya wafanyabiashara waliokua karibu na duka hilo
waliwashauri wafanyabiashara wa tiba asili kujali afya za watumiaji na
sio kuzingatia maslahi binafsi.
walisema uzowefu unaonesha kuwa jamii haina uelewa juu ya dawa hizo hivyo ipo haja kwa ZFDA na baraza la tiba asili kutoa elimu ili kuwasaidia kulinda afya zao.





Post a Comment