BARAZA LA MADIWANI JIJI LA TANGA LAPIGA MARUFUKU STENDI BUBU
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhe. Selebosi Mustafa akizungumza katika mkutano wa baraza la madiwani la robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026 lililofanyika Februari 3, 2026.
..............................
Na Dotto Mwaibale, Tanga
Katika kufanya jitihada za ukusanyaji wa mapato Baraza la Madiwani
la Halmashauri ya Jiji la Tanga, limewataka wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wa abiria katika jiji hilo kutumia
Stendi Kuu ya Mabasi ya Kange.
Hatua hiyo inakuja kufuatia wamiliki wa vyombo vya usafirisha abiria katika jiji hilo kutumia maeneo yasiyo rasmi (Stendi Bubu), kuegesha vyombo hivyo kiholela ndani ya jiji hilo na kusababisha kukosa mapato ambayo yangepatikana kwa kutumia Stendi ya Kange kama ilivyokusudiwa.
Madiwani wa Halmashauri ya jiji hilo kwa kauli moja wameomba mabasi yote ya abiria kuhamia Stendi ya Kange huku wakiomba msaada kutoka kwa Mkuu wa wilaya hiyo Dadi Kolimba.
Mstahiki Meya wa jiji hilo Mhe. Selebosi Mustafa akizungumza katika mkutano wa baraza la madiwani wa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, alisema mpango wa kuhamishia shughuli za usafirishaji katika Stendi ya Kange utachochea uchumi wa Jiji la Tanga.
“Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa kujenga stendi hiyo ulilenga kusaidia kukusanya mapato lakini hadi sasa haujarejesha fedha yoyote kama ilivyotarajiwa,” alisema Mustafa.
“Jambo hili kila wakati tumekuwa tukilizungumzia likiwepo lile la wafanyabiashara wa Tangamano kuhamia sehemu waliyopangiwa sasa ifike mwisho naomba tushirikiane katika jambo hili najua zitakuja ngonjera nyingi hii ni Serikali na ikisema inatakiwa kufuata maelekezo, tunakuomba Mhe. DC utusaidie kulishughulikia mwenzetu una vyombo,” alisema Naibu Meya wa jiji la Tanga Khalid Hamza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Dadi Kolimba alisema kuwa madiwani wa Jiji la Tanga kwa kauli moja wamehazimia kuondolewa kwa mabasi yote yanayoegeshwa kiholela ndani ya jiji na kwenda kuegeshwa Stendi ya Kange ambayo ni maalumu kwa mabasi yote yanayotoka nje ya mkoa wa Tanga.
Kolimba alisema hilo ni jambo zuri lakini changamoto iliyopo mabasi hayo yamekuwa yakiingia moja kwa moja kwenye mitaa ya jiji na kusababisha msululu wa magari na kuondoa utaratibu mzuri uliokuwepo.
“ Jambo hili lilikwisha anza kushughulikiwa kwa vikao ambavyo viliwashirikisha wadau wenye mabasi na kulingana na taratibu za Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), basi lolote linapoingia mjini inapaswa muhusika awe amejenga maegesho yake kwa vigezo vya Serikali na si vinginevyo.
Kwa upande wetu kama kampuni itakuwa imejenga maegesho hayo yenye vigezo hivyo ambayo yatasimamiwe na LATRA wataweza kufikiriwa lakini wale ambao hawata kuwa na maegesho hayo watatakiwa kwenda Stendi Kuu ya Mabasi ya Kange.
“Kama mlivyosikia maazimio ya baraza la madiwani limepanga hadi ifikapo mwishoni mwa Februari ndiyo mwisho mabasi yasiyokuwa na maegesho rasmi katikati ya jiji yawe yamehamia Stendi ya Kange,” alisema Kolimba.
Alisema Serikali itashirikiana na wenye mabasi kufuata utaratibu huo na kweza kuhamia Stendi Kuu ya Mabasi Kange.
Mstahiki Meya wa Jiji hilo Mhe. Selebosi Mustafa akisisitiza jambo kwenye baraza hilo.Naibu Meya wa jiji hilo, Khalid Hamza akichangia jambo kwenye baraza hilo.Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba akizungumza kwenye baraza hilo.Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini akizungumza kwenye baraza hiloDiwani wa Kata ya Maweni Colvas Joseph akichangia jambo kwenye baraza hilo. Diwani wa Kata ya Mabawa, Iddi Samangagho, akichangia jambo.Madiwani wakiwa kwenye baraza hilo.Baraza hilo likiendelea.Madiwani wakishiriki kikao cha baraza hilo.Taswira ya baraza hilo.Wataalam na wakuu wa idara wakiwa kwenye baraza hilo.Wakuu wa Idara na Wataalam wakiwa kwenye baraza hilo.Diwani wa Kata ya Duga, Jafari Mohamed, akizungumza.Naibu Meya Mhe. Khalid Hamza,akipitia nyaraka zake wakati wa baraza hilo.Muonekano wa Jengo la Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990.



Post a Comment