Header Ads

WAIMBAJI WA SIFA NA KUABUDU KANISA LA EAGT WATAKIWA KUJITAMBUA NA KUISHI UTAKATIFU


Makamu Askofu wa  Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Kanda ya Mashariki, Bishop Philimon Phili, akihubiri wakati akifungua Kongamano la Sifa na Kuabudu linalofanyika katika Kanisa la EAGT Sinza Makaburini Mei 27, 2026.

..............................

WAIMBAJI wa Sifa na Kuabudu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Kanda ya Mashariki (KUSK), wametakiwa kujitambua na kuishi maisha ya utakatifu ili kusaidia kuandaa mazingira ya kulihubiri neno la Mungu kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Makamu Askofu wa kanisa hilo Kanda ya Mashariki, Bishop Philimon Phili, wakati akifungua Kongamano la Sifa na Kuabudu linalofanyika katika Kanisa la EAGT Sinza Mei 27, 2026. Kongamano hilo limeandaliwa na Kurugenzi ya Uimbaji wa Sifa na Kuabudu ya KUSK.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Bishop Phili alisema huduma ya kusifu na kuabudu ni muhimu sana ndani ya kanisa na inahitaji watu wenye kujitambua, umoja na utakaso wa kweli.

“Tunataka uamsho. Tunahitaji watu wanaojitambua, walio wamoja na wenye utakaso ndani yao ili ibada ziwe na uwepo wa Mungu,” alisema Bishop Phili.

Alisema huduma ya sifa na kuabudu hufungua njia ya uwepo wa Mungu, hivyo waimbaji wanapaswa kuondoa migawanyiko na vikundi ndani ya kanisa na badala yake kujikita katika kutoa huduma kwa moyo mmoja.

“Anayetaka kuabudiwa ni lazima awapishe Mungu mbele. Kusifu na kuabudu ni ishara ya ushindi kwani mapepo na nguvu za giza hukimbia,” alisema.

Aidha, Bishop Phili alieleza kuwa zamani watu waliogopa hata kupita karibu na makanisa ya kiroho kutokana na utukufu wa Mungu uliokuwapo, lakini akahoji sababu za hali hiyo kupungua katika nyakati za sasa.

“Kwa nini leo nguvu hiyo haionekani kama ilivyokuwa zamani?” alihoji.

Aliwataka wanaohudumu katika idara ya Sifa na Kuabudu kuwa na mioyo safi, unyenyekevu na maisha ya maombi yasiyokoma, huku wakiepuka maneno ya kusengenyana na matendo yasiyoendana na huduma hiyo.

“Kazi hii ni ya Mungu kupitia Roho Mtakatifu, hivyo inahitaji watu wenye maisha safi na wenye kulijua neno la Mungu,” alisema.

Bishop Phili pia aliwataka viongozi wa majimbo wa EAGT Kanda ya Mashariki kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi, akionya kuwa watakaoshindwa kusimamia wajibu wao wataondolewa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Sifa na Kuabudu KUSK Kanda ya Mashariki, Mchungaji Bahati Asumwisye, alisema kongamano hilo limezikutanisha kwaya zote za majimbo ya kanisa hilo pamoja na vikundi vya kusifu na kuabudu na waimbaji binafsi.

Alisema lengo la idara hiyo ni kuwajenga waimbaji katika misingi ya utakatifu, maadili mema na nguvu za Mungu ili waweze kuhudumu kwa ufanisi zaidi.

“Mafunzo haya yanawasaidia waimbaji kuishi maisha matakatifu na kumjua Mungu zaidi. Tunaona kizazi cha sasa kimebadilika na imani potofu pamoja na manabii wa uongo vinaongezeka, hivyo tunawafundisha walinde maadili ya kiimani na kujiepusha na vitendo visivyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Mchungaji Asumwisye.

Naye Katibu wa KUSK Kanda ya Mashariki, Mchungaji Dk. Lukas Dobogo, alisema kongamano hilo la siku nne limehusisha kwaya 27 kutoka majimbo mbalimbali pamoja na vipindi vya mafunzo ya neno la Mungu, maombi ya kiroho na huduma ya uimbaji.

Kongamano hilo lilianza Mei 26, 2026 na linatarajiwa kuhitimishwa Mei 29, 2026 katika Kanisa la EAGT Sinza Makaburini na linaendelea kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi watu wote mnakaribishwa.

Mkurugenzi wa Taifa (KUSK), Mchungaji Gidion Malatila, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Idara ya Sifa na Kuabudu KUSK Kanda ya Mashariki, Mchungaji Bahati Asumwisye, akizungumza katika kongamano hilo.
Katibu wa KUSK Kanda ya Mashariki, Mchungaji Dk. Lukas Dobogo, akielekeza jambo kwenye kongamano hilo.
Viongozi wakuu wa KUSK Kanda ya Mashariki wakiwa kwenye kongamano hilo.Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Sifa na Kuabudu,Mchungaji Bahati Asumwisye na kushoto ni Katibu, .Mchungaji Dk. Lukas Dobogo.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
K9ngamano likiendelea.
Viongozi wakiwa kwenye kongamano hilo. Wa pili kutoka kushoto ni Bi. Ester Bwile.
Kongamano likiendelea.
Viongozi kutoka majimboni wakiwa kwenye kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Idara ya Sifa na Kuabudu KUSK Kanda ya Mashariki, Mchungaji Bahati Asumwisye, akisisitiza jambo kwenye kongamano hilo.
Kwaya ya Beroya kutoka Kibaha, ikiimba.
Kwaya ya Mtende kutoka Kigogo ikiwajibika ipasavyo wakati wa kongamano hilo.
Burudani za kwaya zikiendelea.
Waimbaji wa Kwaya kutoka Jimbo la Kiluvya wakiwa kwenye kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Taifa (KUSK), Mchungaji Gidion Malatila, akielekeza namna ya upigaji wa vyombo vya muziki.
Waimbaji wa Kwaya ya Bethelehem wakiwajibika ipasavyo katika kongamano hilo.
Taswira ya kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Furaha ikitamalaki kwenye kongamano hilo. Kulia ni Mlezi wa Vijana na Mambo ya Kiroho, Leticia Mazimba.
Bi. Ester Bwile akifurahia kongamano hilo kwa jinsi lilivyoandaliwa vizuri.

Hawa ndiyo mabingwa wa kupika chakula chenye ubora wa hali ya juu cha  idadi kubwa ya watu, ndiyo wameandaa chakula cha kusanyiko hilo pamoja na upambaji. Wanapatikana Kanisa la EAGT Sinza Jijini Dar es Salaam kwa mawasiliano piga simu namba 0713080097.

.....................................

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.
 

No comments