KILICHO WAPONZA CHADEMA MBEYA HADI WAKAMATWE HIKI HAPA
MWAKA 1994 hauwezi kufutika katika historia ya dunia baada ya watu zaidi ya
800,000 kupoteza maisha kwa mauaji ya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda.
Wengine zaidi ya 2,000,000 walikimbia nchi na kwenda maeneo mbalimbali duniani
kuomba hifadhi.
Sababu ya yote hayo ni kauli. Wahutu na Watusti walianza kutoleana kauli za
vitisho na kila mmoja kujiona bora zaidi ya mwenzake. Baadaye walichinjana na
kuuana watu wa famailia moja.
Nchini Kenya mnamo mwaka 2007 vurugu baada ya uchaguzi mkuu uliomuweka
madarakani hayati Mwai Kibaki, zaidi ya watau 1,000 walipoteza maisha. Inadaiwa
zaidi ya wanawake 1,200 walibakwa, idadi ya waliojeruhiwa haijulikani na zaidi
ya watu 300,000 walikosa mahali pa kuishi.
Haya yote yalianzishwa na kitu kimoja tu, kauli. Kauli za wanasiasa ni
upanga wenye makali kuliko risasi.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinailalamikia Serikali
inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa haitimizi wajibu wake katika
haki za binadamu. Lakini wanasahau kitu kimoja kuwa wajibu unatimizwa kwa pande
zote mbili.
Mwishoni mwa wiki Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila
alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, juu ya kukamatwa
viongozi wa chama chake na baadhi ya wananchama mkoani Mbeya wakati wakijiandaa
na mkutano wa siku ya vijana waliopanga kuufanya Uwanja wa Ruanda Nzomve mkoani
Mbeya, Agosti 12, 2024.
Awali, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania, Awadh
Juma Hajji alitoa tamko la kuzuia mkutano huo akieleza kuwa kulikuwa na harufu
ya uvunjifu wa amani. Akaagiza pia mabasi zaidi ya 200 yaliyokuwa njiani kutoka
mikoa mbalimbali kwenda Mbeya nayo yazuiwe.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, Moza Ally alitoa tamko vijana
wote waliokuwa njiani kwenda Mbeya kwa mabasi wazime magari wafunge barabara
ili kusitisha shughuli zote siku ya Jumamosi na Jumapili yaani Agosti 10 na 11,
2024.
Mambo haya yanaendana kinyume kabisa na kauli za pamoja zilizotolewa
Januari 2023, Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam wakati Rais Dk. Samia
Suluhu Hassan alipowaita viongozi wa vyama vyote vya siasa vyenye usajili
nchini kuzungumza nao, ambapo hadi viongozi wa Chadema walihudhuria.
Siku hiyo Rais Samia alikutana na vyama vya siasa nchini ambapo mbali ya
mambo mengine alimaliza kifungo cha takriban miaka sita kilichowekwa na
mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli juu ya mikutano ya vyama vya siasa.
Aliruhusu siasa za majukwaani zifanyike, lakini alitoa angalizo kuwa uhuru
una mipaka yake na haki inaendana na wajibu. Hivyo, siasa za majukwaani
zifanyike kwa ustaarabu na kutumia lugha za staha. Si matusi wala
kudhalilishana.
“Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano
ya hadhara, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza, lile tangazo la
kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka,” alisema Rais Samia na kusisitiza:
“Lakini ndugu zangu tuna wajibu, wajibu wetu serikali ni kulinda mikutano
ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni
zinavyosema, twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, tukafanye siasa za kupevuka,
tukafanyeni siasa za kujenga si za kubomoa, sio kurudi nyuma hapa tulipofika,
sisi ndani ya CCM tunaamini katika kukosolewa na kujikosoa.”
Kwa mtu muungwana na mwenye nia njema na nchi yake, haya maneno yangetosha
kuwa mkataba wa amani kwa wakati wote nchini.
Lakini zuio la Jeshi la Polisi linatokana na kauli za viongozi wa BAVICHA,
ikiwemo hizi:
“Kama kijana yeyote unayeipenda nchi yako ya Tanzania umeshalia miaka yako
yote, siku hiyo ya Agosti 12, 2024 tunakwenda kuweka hatma ya taifa letu la Tanzania
mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo Uwanja wa
Ruanda Mzomve, Mbeya.
“Tupo Serious na jambo hili, kwa hiyo vijana wote wa CHADEMA kama ambavyo
vijana wa Kenya wamejitambua siku ya Tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja
kwa serikali, vijana wa Kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa
serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.”
Kauli kama hizi si za kuzipuuza, Tanzania ni moja ya mataifa yanayosifiwa
kwa utulivu. Yanayosifiwa kwa amani na kila lililo jema. Haiwezekani watu
wachache wenye nia ovu wavuruge misingi imara ya taifa hili iliyojengwa na
watangulizi wetu.
Hakuna mahali vyama vya siasa vimezuiwa kufanya siasa. Tumeshuhudia
viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini wakizungumza kwenye majukwaa kwa nyakati
tofauti, tangu kufunguliwa mikutano ya hadhara.
Iweje Jeshi la Polisi libadili kauli yake? Unadhani Jeshi la Polisi
linaweza kukiuka amri ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais
Dk. Samia Suluhu Hassan?
Ni wazi lipo jambo haliko sawa kiusalama. Hatua sahihi lazima zichukuliwe
kwa wakati kabla mambo hayajaharibika.




Post a Comment