SOS CHILDRENS VILLAGES TANZANIA YAZINDUA MRADI KUSAIDIA WATOTO WANAOFANYA KAZI MITAANI
Viongozi wa Shirika la SOS Children's Villages Tanzania na Wadau mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kuzindua Mradi wa Kuwasaidia Watoto Waishio na Kufanya Kazi Mitaani Jijini Arusha Juni 8, 2026.
......................................
Na Ahmed Mahmoud, Arusha
SHIRIKA la SOS Children's Villages Tanzania limezindua rasmi mradi wa kuwasaidia watoto waishio na kufanya kazi mitaani nchini, unaotekelezwa katika mikoa mitano na wilaya 17, ukiwa na lengo la kuwafikia zaidi ya watoto 4,200.
Mikoa inayotekeleza mradi huo ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza na Pwani, ambapo unalenga kuboresha ustawi wa watoto walioko katika mazingira hatarishi kupitia huduma za ulinzi, elimu, afya na ushauri nasaha. Katika Mkoa wa Arusha, mradi huo unatekelezwa katika Wilaya ya Arusha Jiji na Arumeru, na unatarajiwa kuwafikia zaidi ya watoto 750.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha watoto wanapata ulinzi, malezi na haki zao za msingi katika mazingira salama.
Alisema watoto waishio na kufanya kazi mitaani hukumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu, huduma za afya, malezi duni na ukatili, hali inayohitaji juhudi za pamoja kutoka kwa serikali, jamii na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Apolinar Seiya, alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika kutatua changamoto za watoto waishio na kufanya kazi mitaani kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi.
Alisema watoto hao hukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa malezi bora, elimu na ulinzi, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu wa jamii na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha wanarejea katika mazingira salama ya familia na kupata huduma stahiki.
Mkurugenzi wa SOS Children's Villages Tanzania, Thomas Kipingili, alisema mradi huo unalenga kuwaondoa watoto katika mazingira hatarishi na kuwaunganisha na familia zao pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto katika jamii.
Alieleza kuwa shirika linatumia mbinu za kijamii ikiwemo michezo, sanaa na mazungumzo ya kijamii kuwasaidia watoto waliozoea maisha ya mtaani kubadilika na kuzoea maisha ya kifamilia na jamii. Alisisitiza kuwa mafanikio ya mradi huo yanategemea ushirikiano wa pamoja kati ya serikali, jamii na wadau mbalimbali katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na endelevu.
Picha zaa matukio mbaalimbali wakati wa uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.












Post a Comment